Saturday, January 12, 2019

TUJIKUMBUSHE HISTORIA YA MAPINDUZI YA ZANZBAR

Tarehe kama ya leo ya mwaka 1964, takribani miaka 55 imekwishapita. Taifa la Tanzania na watanzania wote kwa jumla wanayakumbuka mapinduzi matukufu ya Zanzibar, ambayo yalitekelezwa usiku wa siku ya tarehe 12/01/1964.

Na kama inavyofahamika wazi, kuwa ni Mapinduzi. Kwa maana hiyo ni wazi kuwa kuliwapo na serikali ama mfumo wa kiutawala, na ambao ni utawala huo ndio uliopata kupinduliwa katika mapinduzi hayo ambayo yalitekelezwa na vijana wa chama cha Afro-Shirazi Party (ASP).

Kwa hiyo tunapoiadhimisha siku hii ya leo, ni vema tukafanya kumbukizi kwa ufupi; ili kuweza kuona chanzo cha  mapinduzi, jinsi hali ilivyokuwa, na wahusika wa mapinduzi hayo, na ambao walipinduliwa.

Historia Fupi ya Siasa za Zanzibar:

Mnamo 1939 chama cha Shirazi Association (SA) kilianzishwa, kwa madhumuni hasa ya kutetea na kupigania haki za watu wa jamii ya Shirazi. Na ikumbukwe kuwa tangu wakati huo ambapo SA kinaanzishwa chama cha African Association (AA) kilipata kuwapo tayari, kwani ni mwaka 1930 ndipo kilianzishwa. Na mwaka 1948 AA kilibadili jina na kutambulika kwa jina la Zanzibar African Association (ZAA).

Na kwa kuwa lengo kuu katika harakati za ZAA na  za SA, ni kutafuta uhuru wa watu wa Zanzibar kwa maana ya washirazi na waafrika; ili kuepuka makucha ya wakoloni. Vyama hivi vikaamua kuungana ili kuongeza nguvu katika kukamilisha adhima hiyo, hivyo ASP ikaazaliwa katika mwaka wa  1957. Na Mwenyekiti wake wa kwanza alikuwa Sheikh Abeid Amani karume na Katibu Mkuu wake  alikuwa  Sheikh Thabit Kombo.

Chanzo cha Mapinduzi:

Ijapokuwa ASP kiliendelea na majukumu yake na harakati zake za kuutafuta uhuru, ni wazi kuwa kilikutana na upinzani wa mara kwa mara kutoka kwa serikali ya mkoloni, chama ZPPP na chama ZNP. Hata hivyo siku ya 10.12. 1963 Zanzibar ikapata kuwa huru kutoka kwa Waingereza. Na ikabakia katika utawala wa Sultan Jeshmid bin Abdallah Al Said na Waziri Mkuu wake alikuwa ni Mohamed Shamte.

Hata hivyo uhuru huo haukuchukuliwa kuwa ni uhuru kamili kwa wanachama wa ASP, ambapo wanachama wake wengi walikuwa ni waafrika! Kwani uhuru huo haukuwa na kusudi hasa na watu wanyonge ambao wamekuwa wakionewa na kunyonywa na kukandamizwa. Na ukizangatia kuwa kuliwapo na uonevu kwa ASP katika matokeo ya chaguzi ambazo zilipata kufanyika katika mwaka wa 1963.

Hali ilivyokuwa:

Kwa jinsi hiyo basi, kwa nyakati tofautitofauti vijana wa ASP wakiongozwa na Mwenyekiti wao Sheikh Amani Karume, walianza kufikiri na kuratibu mipango ya kuhakikisha kuwa wanafanikiwa kuipindua serikali ya Sultani. Katika jopo hilo walikuwapo pia; Abdulrahman Babu, raia mmoja wa uganda aliyefahamika kwa majina ya John Okello, Saleh Sadaalah, Idris Wakyl, Kassim Hanga, Othaman Sharif na wengine wengi vijana ambao walishiriki moja kwa moja kuteka vituo vya polisi, katika harakati za mapinduzi hayo.

Na hata ulipofika usiku wa tarehe 12/01/1964, adhima hiyo ya mapinduzi ikawa imetimia. Na mara baada ya mapinduzi hayo, sulatni Jemshid alitorokea na kwenda Uingereza, na kuiacha Zanzibar katika uangalizi wa chama cha ASP. Na baada ya siku chache Mwenyekiti wa ASP Sheikh Abeid Karume akiwa kama mwenyekiti wa baraza lililofanikisha mapinduzi hayo, akachukua nafasi ya Rais wa Zanzibar, na alidumu kwenye nafasi hata kifo chake siku ya 07/04/1972.

Kwa hiyo, tunapoiadhimisha siku hii ya Mapinduzi yaliyofanyika miaka 55 iliyopita ni wazi kuwa kwa wakati mmoja tunajifunza hali ya kupenda kuwajibika katika hali ya uzalendo na uadilifu wa kweli; na kuwa tayari kujitoa kwa ajili ya kupigania maslahi ya watu wanyonge.

Ninawatakia maadhimisho mema ya siku ya Mapinduzi ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment